Thursday, July 18, 2013

MWANAFUNZI JELA MIAKA 7 KWA KUIBA BODA BODA

 

Na Elizabeth Ntambala wa matukiodaima.com ,Sumbawanga

MAHAKAMA ya wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa,imemuhukumu kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka saba jela Emmanuel Costantino(20) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Mtakatifu Maurus iliyopo mjini  Sumbawanga kwa kosa la wizi wa pikipiki.

Akisoma hukumu  hakimu wa mahakama hiyo Adamu Mwanjokolo alisema kuwa mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo pasipo kuwa na shaka na  imetoa adhabu hiyo kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa na tabia mbaya za wizi kama alivyofanya mtuhumiwa.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa polisi mkaguzi msaidizi Thomas Kilakoi kuwa mnamo Oktoba 28 mwaka jana mtuhumiwa alikodi pikipiki aina ya Sanya yenye namba za usajili T 874 BYT  yenye thamani ya shilingi 1,800,000 mali ya Brassy Kaozye na kudai kuwa anakwenda kijiji cha Mfinga kumfuata baba yake ili ampe ada aje alipe kwani anadaiwa shuleni.

Baada ya kukabidhiwa pikipiki hiyo mwanafunzi huyo alitoroka nayo na kukimbilia Ifakara mkoani Morogoro ambapo alianza kutafuta mteja ili aiuze kutokana na kuamini kuwa yupo sehemu salama na amefanikiwa kuikwepa mikono ya dola.

Kutokana na jeshi la polisi kumfuatilia mtuhumiwa kwa kutumia mitandao ya simu walifanikiwa kumkamata mwezi mmoja baadaye akiwa Ifakara na pikipiki hiyo huku akihaha namna ya kuiuza kutokana na kuchelewa kupata mteja,ndipo alipokamatwa na kurudishwa mkoani Rukwa na kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment