Wednesday, July 17, 2013

MBINU ZA KURUDISHA KIBURUDISHO CHAKO CHA ZAMANI


KAMA siyo Mungu, tusingekutana tena leo katika ukurasa huu wa kirafiki ambao unatuweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuishi maisha ya amani na upendo na wenzi wetu.

Ndugu zangu, kama ukitaka kufanikiwa basi ishi kwa upendo na wenzako. Uwe na furaha muda wote, shirikiana na wenzako na penda zaidi majadiliano kuliko uamuzi wa peke yako ambao mara nyingi husababisha matatizo.
Nimesema hivyo kwa sababu kuna baadhi ya watu wenye tabia hizo. Upendo ndiyo msingi wa kila kitu katika maisha. Ukiwapenda wenzako, hata milango ya riziki hufunguka.
Nazungumza na wale ambao wameachana na wenzi wao kwa sababu mbalimbali lakini baada ya kujichunguza kwa muda, wamegundua kwamba bado wana nafasi katika mioyo yao. Wanataka kuwarudisha.
Hilo si jambo baya hata kidogo. Kuna wakati fulani niliwahi kufundisha kuhusu namna ya kuachana na mwenzi ambaye umegundua kwamba hakufai.
Baadhi ya watu walishangaa na kwa kweli nilipokea simu nyingi sana za watu wakilaumu na wengine wakitaka kupata elimu zaidi; kwa nini nazungumzia kuhusu watu kuachana?
Ukweli ni huu; unaweza kuwa na mtu kwa muda fulani, ukagundua kumbe ulikuwa naye kwa sababu ya tamaa zako tu na si kweli kwamba unampenda kwa dhati ya moyo wako. Je, ikiwa hivyo ni sahihi kuendelea kumpotezea muda mwingine ili hali unajua kuwa huna haja naye?
Yes! Kutoka hapo sasa ndipo tunapoweza kujadili mada hii, kwamba umeachana na mwenzako kwa muda mrefu. Huenda ilikuwa hasira au kupishana maneno lakini baada ya kujichunguza kwa muda, ukagundua kwamba bado nafasi yake ipo katika moyo wako.
Katika mtindo huo ni sahihi kabisa kurudiana na mwenzi wa aina hiyo. Nilishaeleza mengi katika matoleo mawili yaliyopita, leo nakwenda kuhitimisha. Twende tukaone...

MTOKO
Kutokana na ukaribu wenu, kumwalika katika mtoko wa chakula cha mchana au usiku, haitakuwa vigumu kwake. Hiyo itakuwa njia nyingine ya kumfanya awe karibu yako zaidi.

Mkiwa katika mtoko huna haja ya kuzungumza chochote kuhusu uhusiano wenu, labda kama yeye ataanzisha mjadala huo. Ongelea mambo mengine ambayo ni maarufu zaidi labda katika duru za siasa, sanaa n.k lakini si mambo yanayohusu mapenzi kabisa.

Kama kichwani mwake alikuwa amekufanya kama rafiki yake wa kawaida, mtazamo utaanza kubadilika taratibu na kuanza kutamani kurudi tena mikononi mwako. Jaribu kufikiria, kama umetoka naye, akiamini labda unataka kumuomba msamaha na kurudiana naye, wewe unaanza stori za soka! 
Bila shaka atajiona kama mpumbavu kichwani, si ajabu akaamua kujifunga mwenyewe kwa kuomba urudi tena kwake.



SASA JADILINI PAMOJA
Hatua hii ndiyo muhimu zaidi. Sasa unatakiwa kuanza kuzungumzia juu ya uhusiano wenu. Mwambie jinsi ulivyokuwa ukifurahishwa na mapenzi yenu. Msifie alivyokuwa anajua majukumu yake na kukuonesha mapenzi ya dhati.

Si vibaya kama utamweleza pia sababu ambazo unahisi zilisababisha wewe na yeye kuachana. Kwa kauli hizo utampa nafasi ya kuchambua/kumjua mwenye makosa na mahali pa kurekebisha.

KIRI MAKOSA YAKO
Ikiwa kuna mahali unaamini ulikwenda kinyume na yamkini ndiyo sababu kuu iliyosababisha muachane, kiri makosa yako mbele yake. Mweleze kwamba wewe ndiyo chanzo cha matatizo na huenda kama si kukosea, msingeachana.

Kujutia hasa kama uso wako utawakilisha vyema kilicho moyoni mwako, kutamfanya akuone muungwana ambaye unatambua ulipojikwaa na sasa unataka kurekebisha makosa yako. Hapo utakuwa na nafasi kubwa ya kumnasa kwa mara nyingine.


MWELEZE YAKO YA MOYONI

Sasa huna sababu ya kuendelea kujitesa, KAMA MUDA WOTE HUO HAJASEMA CHOCHOTE, sasa toa dukuduku lako. Mwambie moja kwa moja kilichopo moyoni mwako.
Kwamba unahitaji nafasi nyingine kwake, maana umeshajua makosa yako. Hii ni nafasi ambayo si rahisi kabisa kuchomoka. Itumie vilivyo. Sauti yako pekee itoshe kumaanisha kile kilichopo moyoni mwako.
Lazima atakuelewa.
Kama utakuwa umefuata kwa makini vipengele vyote hapo juu, lazima urudi tena mikononi mwake. Kuna nini tena? Ameshakuwa wako huyo, ila kuwa makini usimpoteze tena.

AKIKATAA JE?
Pamoja na kufuata vipengele vyote hivyo, inawezekana akakataa. Kukataa kwake lazima kuna sababu nyingi. Mwingine anaweza kukuambia moja kwa moja sababu za kukataa kurudiana na wewe wakati mwingine anaweza asiseme chochote.
 Huenda akakuambia kwamba tayari ana mtu wake, au hafikirii kurudi mikononi mwako; usihuzunike.
Ni bora sana huyu anayekuambia ukweli, kuliko kurudi halafu ukutane na mateso yaleyale. Inawezekana labda hana mapenzi na wewe. Kama ndivyo, kuna sababu gani ya kujikomba? Kubaliana na ukweli, halafu subiri mwingine!
Sikia...subiri na siyo utafute, maana mwenzi wa kweli huja mwenyewe, hatafutwi! Upo hapo rafiki?

No comments:

Post a Comment