Viongozi
wa dini wamewataka waumini kote nchini kulinda amani na umoja uliopo
ili nchi isije ikaingia kwenye mgawanyiko wa kidini na kuleta machafuko
hapa Tanzania. Wito
huo umetolewa na viongozi wa dini leo Ikulu ya Dar-Es-Salaam mara baada
ya kikao cha pamoja baina ya viongozi wa dini na Rais Jakaya Kikwete. Viongozi
hao wa dini wamefika leo wakiongozwa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa,
ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Viongozi wengine wametokea Baraza la Kikristo Tanzania (CCT) Seventh Day Advertist (SDA) na Baraza la Pentekoste Tanzania (PCT).
Viongozi wengine wametokea Baraza la Kikristo Tanzania (CCT) Seventh Day Advertist (SDA) na Baraza la Pentekoste Tanzania (PCT).
Mkutano
huo umeanza kwa Askofu Ngalalekumtwa kusoma tamko lao la pamoja kwa
Rais Kikwete ambalo ndilo limetoa muongozo wa mazungumzo hayo ya leo
ambayo yamehusu Amani na Usalama wa Taifa na migogoro ya kidini ndani ya
jamii.
Mkutano wa viongozi wa dini ya Kikristo Tanzania ni mojawapo ya jitihada
za Rais Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa hali ya
sintofahamu ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.
“Nataka tuzungumze ni namna gani tunaweza kutoka kwenye hali hii na
tunakwendaje mbele zaidi na kuhakikisha nchi yetu bado inakua ya amani
na umoja kama ilivyozoeleka” Rais amesema na kutoa nafasi kwa viongozi
wa dini kutoa maoni yao.
Viongozi hao wa dini wamemueleza Rais Kikwete kuwa wanaunga mkono
jitihada zake za kutafuta amani na kwa pamoja wamekubaliana uandaliwe
mkutano wa pamoja baina ya viongozi wa dini zote ambapo masuala ya amani
na umoja wa nchi utajadiliwa kwa kirefu.
Katika kikao cha leo pande zote zimekubaliana kuwa kuna changamoto
zilizoko sasa zinahitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili kuepusha
nchi kutumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi, na pia kukubaliana kuwa
pande zote, kwa maana ya serikali na taasisi za dini, zinawajibu mkubwa
wa kuhakikisha amani inadumu.
Kabla ya kikao cha leo , Rais amewahi kukutana na viongozi wa dini ya
kiislamu na kikristo mmoja mmoja ambapo alikua akitafuta maoni na
ushauri wa pande zote kabla ya pande zote hazijakaa pamoja na kuwa na
msimamo wa pamoja.
Kikao cha leo kimehitimisha jitihada hizo na kinachofuata ni mkutano
mmoja ambapo Rais Kikwete atakutana na viongozi wa dini zote kwa pamoja
hivi karibuni.
………...“MWISHO”……..
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu-DSM
23 Aprili, 2013
Picha zaidi angalia hapa chini
Rais Kikwete akisalimiana na viongozi wa
madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Ikulu jijini Dar es salaam leo
ambapo amekuwa na mazungumzo nao ikiwa ni mojawapo ya jitihada za Rais
Kikwete kutafuta muafaka na kutafuta utatuzi wa hali ya sintofahamu
ambayo inanyemelea nchi yetu katika kipindi hiki.
Rais Dk Jakaya Mrisho Kikwete akiwa
katika mkutano na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo
alipokutana nao leo April 23, 2013 Ikulu jijini Dar es salaam katika
kukutana na makundi mbalimbali ya kidini ili kuondoa changamoto za
kiimani zilizojitokeza nchini hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment