Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akikaribishwa rasmi kwenye mkutano wa "High
Level Group" na Dr. Sheila Tlou, Mkurugenzi wa UNAIDS Regional Support
Team kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika katika siku ya pili ya
mkutano huo unaofanyika jijini Gaberone nchini Botswana tarehe
31.7.2013.
Baadhi
ya wajumbe wa mkutano wakisoma jarida linalochapishwa na Taasisi ya
Wanawake na Maendeleo, WAMA, huku wakiendelea na mkutano.
Mke wa
Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo Mama Salma
Kikwete akifunga rasmi mkutano wa High Level Group uliokuwa unafanyika
kwenye hoteli ya Lasmore nchini Botswana tarehe 31.7.2013.
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akifanya mazungumzo na Profesa Alaphia Wright,
Mwakilishi wa UNESCO kwenye nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika mwishoni
mwa mkutano wa siku mbli wa High Level Group ulikuwa ukifanyika jijini
Gaberone nchini Botswana tarehe 31.7.2013.
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akimsikiliza kwa makini Dr. Patricia Machawira,
Mshauri wa HIV na AIDS kwa nchi za ukanda wa Mashariki na Kusini mwa
Afrika mwishoni mwa mkutano wa siku mbili uliokuwa unafanyika nchini
Botswana. Dr. Machawira alikuwa akimshukuru Mama Salma kwa ushiriki wake
kwenye mkutano huo uliofanyika tarehe 30.7 hadi 31.7.3013.
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akihojiwa na na MS Sandra Chuma kutoka kwenye
sekretarieti ya High Level Group, kuhusu masuala mbalimbali
yanayowakabili wanafunzi yanayohusiana na elimu na afya, mwishoni mwa
mkutano.
Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete akiagwa rasmi na Mwakilishi wa UNESCO wa Kanda
ya Kusini mwa Afrika Profesa Alaphia Wright nje ya hoteli ya Lasmore
huko Gaberone nchini Botswana ulikofanyika mkutano wa siku mbili wa High
Level Group kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kuhusiana na
elimu na afya kwa vijana.
PICHA NA JOHN LUKUWI.
Na Anna Nkinda- Gaborone, Botswana
Imeelezwa
kuwa watoto wa kike wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za
udhalilishaji na unyanyasaji wa jinsia, ukosefu wa elimu, utaalamu na
huduma zitakazowasaidia kukaa shuleni , kujikinga na mimba za utotoni
,ugonjwa wa Ukimwi na virusi vinavyosababisha kansa ya shingo ya kizazi.
Hayo
yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifunga
mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya
afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki
(EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika katika Hoteli ya Lansmore Masa
Square iliyopo mjini Gabarone nchini Botswana.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema ingawa upatikanaji wa huduma na mahitaji ya vijana ni
madogo katika nchi nyingi za kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika
bado kuna tofauti kubwa ya utolewaji wa huduma hizo kwa vijana wa kike
ukilinganisha na wa kiume ambao wao wanapata zaidi.
Alisema
kwa kufanya kazi kwa pamoja kati ya mashirika yanayofanya kazi chini ya
mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (UN) na mashirika ya kijamii wanaweza
kutambua mahitaji na changamoto zinazowakabili vijana na kuwaomba
wakati wanakusanya maoni wawashirikishe viongozi na jamii nzima.
“Tunachotakiwa
kufanya kama wanakamati ni kutumia muda tuliopewa kusoma ripoti yote na
kuielewa kisha kuwashirika wadau mbalimbali wa wa maendeleo ili waweze
kujadili ripoti hii na kutoa maoni yao”, alisema Mama Kikwete.
Akimkaribisha
Mama Kikwete kufunga mkutano huo Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na
Kusini mwa Afrika kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na
Ukimwi (UNAIDS) Prof. Sheila Tlou alimshukuru kwa kukubali kwake kuwa
mmoja wa wanakamati kwani yeye ni kinara kati ya wake wa marais wa
Afrika katika suala zima la kupambana na ugonjwa wa Ukimwi na kumsadia
mtoto wa kike.
Alisema
kuwa miaka ya nyuma Umoja wa Mataifa (UN) ilikuwa inafanya kazi na kila
mtu aliyekuwa na mamalaka lakini hivi mashirika yote yaliyopo chini ya
UN yanafanya kazi kwa ushirikiano na hivyo kuzisaidia nchi husika
kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
“Kwangu
mimi hii ni historia kwani mpango kazi wa Maputo (Maputo Plan of
Action) na makubaliano haya ya leo yatasaidia kushughulikia utolewaji
wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kwani jambo hili
linatakiwa kuangaliwa kwa umakini zaidi hakika tutafanya kitu katika
jamii yetu kwakuwa vijana wanakabiliwa na matatizo mengi ndani ya nchi
zetu”, alisema Prof. Tlou.
Akisoma
taarifa ya makubaliano ya kamati hiyo Afisa Programu kutoka UNESCO
Dhianaraj Chetty alisema kuwa kabla ya kuandaa ripoti hiyo walikusanya
mawazo ya wadau mbalimbali kutoka nchi 21na kuandika ripoti kuhusu
Vijana wa leo wako tayari kwa kesho? na kuangalia matatizo
yanayowakabili na kugundua mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuimarishwa kwa upatikanaji wa elimu.
Pia
katika ripoti hiyo kamati iliangalia kiwango cha uelewa wa maambukizi
mapya ya ugonjwa wa Ukimwi kwa baadhi ya nchi wanachama na faida za
utoaji wa huduma kwa vijana wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).
“Uelewa
wa ugonjwa wa Ukimwi kwa vijana ni chini ya asilimia 40, wasichana
wanahangaika kupata na kumaliza elimu ya Sekondari, na kati ya
wasichana 52 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 wanapata maambukizi
mapya ya Ukimwi kwa kila saa moja katika kanda.
Kuna
idadi kubwa ya upatikanaji wa mimba zisizohitajika na utoaji mimba usio
salama, hii ni changamoto ya dharula ambayo inatufanya sote kuangalia
jinsi gani tutapata nafasi ili tuweze kubadilisha na hali hii leo na
siku za baadaye”, alisema Chetty.
Makubaliano
hayo yanaangalia kazi ambazo wanachama wa SADC na EAC wanafanya ili
kuangalia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana
yatapelekwa kwa wadau wote, vijana na mawaziri wa wizara za Afya na
Elimu na kutoa mawazo yao kuanzia mwezi wa nane hadi wa kumi mwaka
huu.
Mwezi
wa kumi na mbili kamati hiyo itakutana kabla ya kufanyika kwa mkutano wa
kimataifa wa vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na magonjwa ya zinaa ambao
utafanyika mjini Cape town nchini Afrika ya Kusini na kupitisha
makubaliano hayo (document) kisha yatasainiwa na mawaziri husika
katika mkutano huo ambayo itakuwa ni sehemu ya utekelezaji kwa nchi.
Mkutano
huo wa siku mbili uliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kupamba na Ukimwi (UNAIDS) , UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia watoto (UNICEF), Shirika la Chakula Duniani (WHO),
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Sayansi na Utamaduni
(UNESCO) lengo kuu likiwa ni kuhakikisha kuwa vijana wote wanapata
elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia jambo ambalo litawasaidia
waweze kufahamu zaidi ugonjwa Ukimwi.
No comments:
Post a Comment