Imeandikwa na Albert Sanga, Iringa
Miezi
kadhaa iliyopita kupitia Redio TBC Taifa, ofisa mmoja wa Wizara ya
Maliasili na Utalii aliulizwa swali hili, "Je, inawezekana watu binafsi
kufungua mashamba ya miti na kufanya biashara ya kuuza miti ya mbao?"
Ofisa huyo alijibu hivi, "...inaruhusiwa...hata mimi najilaumu kuwa
miaka ile wakati tunapanda msitu wa serikali kule Mufindi mimi
sikukumbuka kutafuta maeneo kwa wenyeji nikapanda miti. Kama ningefanya
hivyo nadhani leo na mimi ningekuwa milionea". Mahojiano yale....SOMA ZAIDI
yamenipa hamasa ya kuileta makala hii wiki hii.
Tangu
mwanzoni mwa mwaka huu nimekuwa nikiandika makala za hamasa na ujenzi wa
fikra kuhusu mitazamo yetu na uthubutu wa kufanikiwa kupitia biashara.
Nikiamini kuwa wengi mmeshajenga mitazamo chanya na utayari kuhusu
biashara na uwekezaji, sasa nachukua hatua mpya.
Hatua hii
ni ya kuonyesha na kuchambua tija (pay offs) za fursa mbalimbali za
kibiashara. Hadi kufika mwishoni mwa mwaka huu nimepanga kuwashirikisha
fursa takribani kumi pamoja na utaratibu maalumu wa kuwasaidia wote
watakaohitaji kuzichangamkia fursa hizo. Fursa nayoanza nayo leo ni hii
ya kilimo cha miti.
Nitakueleza
kila kitu ikiwamo, hali ya biashara hiyo kwa sasa na miaka ijayo,
gharama na hatua za kuanzisha biashara hiyo, na usimamizi wa biashara
hii. Na mwisho kabisa nitakueleza jinsi nilivyojipanga kukusaidia wewe
utimize ndoto yako ya kumiliki mashamba ya miti ikiwa utahitaji kufanya
hivyo.
Kilimo
cha miti kimepata umaarufu wa ghafla miaka ya hivi karibuni kutokana na
sababu mbalimbali ikiwamo ya ongezeko la mahitaji ya mazao ya miti na
changamoto ya mazingira. Katika Tanzania, Mkoa wa Iringa ni moja ya
mikoa maarufu inayoongoza kwa misitu mikubwa ya kupandwa. Miti inatumika
kwa mbao, nguzo za umeme, nguzo za kujengea nyumba na utengenezeaji wa
karatasi.
Ukiacha
mahitaji haya tuliyoyazoea hivi sasa kumeibuka fursa nyingine mpya
ambako mashirika ya kimazingira kutoka Magharibi yananunua hewa ukaa
(carbon dioxide). Kwa maana hiyo unaweza kupanda shamba la miti halafu
ukawa unakusanya dola kwa kuuza hewa ukaa wakati ukisubiri miti ikomae
uvune mbao, nguzo au miti ghafi ya kutengenezea karatasi.
Binafsi
niliichangamkia biashara hii miaka minne iliyopita na 'I'm real serious
with it'. Nimejiwekea lengo la kupanda ekari 20 kila mwaka. Kilimo hiki
cha miti ni uwekezaji wa muda wa kati na mrefu (middle & long term
investments). Kiutamaduni Watanzania wengi huwa hawavutiwi na uwekezaji
wa muda mrefu.
Hata
hivyo, kama una mpango wa kuwa na baadaye imara kiuchumi usikwepe
kufikiria uwekezaji wa muda mrefu. Waingereza husema "Information is
power". Wengi hawajachangamkia fursa hii kwa kukosa taarifa tu. Kazi
yangu leo ni kukupa taarifa hizi za utajirisho.
Ekari
moja ya shamba inachukua wastani wa miti 600. Wastani wa chini wa mti
mmoja kwa sasa uliokomaa ni Sh 20,000. Ina maana katika ekari moja ukiwa
na miti iliyokomaa unakusanya Sh milioni 12. Fedha hiyo (kadirio la
chini kabisa) utaipata ikiwa unaamua kuuza kwa bei ya jumla miti ikiwa
shambani. Lakini kama ukiamua kupasua mbao wewe mwenyewe unaweza kuvuna
mbao hadi za 25,000,000 kwa ekari moja.
Gharama
ya kununua shamba tupu ni kati ya Sh 200,000 hadi Sh milioni moja
kutegemea na maeneo husika unayotaka au kupata. Gharama za kuandaa
shamba, kununua miche na kupanda ni kati ya Sh 400,000 hadi Sh 600,000.
Hii ina maana unaweza kumiliki ekari moja ya msitu wa miti kwa hadi Sh
600,000 tu.
Kilimo
cha miti ni rahisi sana kwa sababu ukishapanda hakihitaji uangalizi
mkubwa sana na wala hauhitajiki uwe karibu na shamba/mradi muda wote.
Kuna kazi chache ambazo zinahitajika ukishapanda shamba lako. Mvua
inyeshe au isinyeshe mti wa mbao, nguzo au karatasi ukishachipua huwa
haufi kwani huendelea kutumia unyevu wa ardhini.
Kazi
namba moja unapokuwa umeshakamilisha upandaji wa miti kwenye shamba, ni
kutengeneza njia za kuzuia moto walau mara moja kwa mwaka. Kazi ya pili
ni kufyekea miti inapokua walau kwa mwaka mara moja. Gharama zote hizo,
yaani kutengeneza njia za moto, kufyekea na kulinda moto haizidi Sh
200,000 kwa mwaka mzima.
Miti
hukomaa kuanzia miaka sita hadi 10 kutegemea na utunzaji unaoufanya. Hii
ina maana kuwa ukichukua Sh 200,000 unazogharimia shamba kila mwaka
ukazidisha mara sita unapata Sh 1,200,000.
Kwa maana
hii gharama za kuhudumia shamba la miti ekari moja kutoka kupandwa hadi
kuvunwa ni kati ya Sh milioni 1.2 hadi Sh milioni mbili. Ukichanganya
na gharama ya kupata ardhi na kupanda miti yenyewe unapata kuwa gharama
nzima hadi unavuna ni kati ya Sh 2,000,000 kwa kadirio la chini.
Hapa ili
kuokoa nafasi nimeweka makadirio yaliyochanganya milinganyo ya muda wa
kuvuna, eneo unalopata pamoja na thamani ya fedha katika muda husika.
Gharama hizi ninazopiga ni ikiwa utaamua kununua shamba leo na kama
ungekuwa tayari una shamba ambalo unalihudumia leo.
Hata
hivyo, nadhani wote tunafahamu kuwa ardhi ni rasilimali inayopanda
thamani kila siku. Vile vile tunatambua kuwa suala la mazingira ni tete
kwa sasa na katika karne zijazo kama wataalamu wanavyotuthibitishia. Hii
ina maana kuwa ukiwa na shamba la miti leo, thamani ya ardhi hiyo
inazidi kupanda kila siku na miti uliyopanda inazidi kupanda thamani
kila kukicha.
Jambo la
uhakika ni kuwa hata kama bei ya miti, mbao, nguzo itayumba hutaweza
kupoteza mtaji uliotumia na wala hutakosa kuzalisha faida kwa shamba
utakalokuwa umemiliki, iwe ni eka moja, kumi, mia au elfu moja. Mbali na
hivyo unaweza ukaona, ahaa, miaka sita hadi 10 ni mingi mno; bado una
nafasi ya kupata faida hata ndani ya mwaka mmoja, miwili na kadhalika.
Ukishapanda
shamba la miti ekari moja kisha baada ya mwaka mmoja ukaamua uuze
utauza si chini ya milioni mbili hadi nne. Kukusanya milioni nne kwa
mtaji wa laki sita, pasipo kutumia muda mrefu au usumbufu wa kusimamia,
hakika ni faida nono.
Huenda
hadi kufika hapa unaweza ukawa umeshavutiwa na biashara hii. Wengi wenu
mnaweza kujiuliza maswali makubwa mawili; "Ninatamani nifanye mradi huu,
lakini Iringa sikufahamu na hata kama nakufahamu nitaanzia wapi kupata
hayo maeneo?" Pili, "Niko mbali na sina muda wa kushinda Iringa, je, ni
nani atanisaidia kupanda, kusimamia na kuendesha hayo mashamba?"
Kama si
hayo maswali mawili hapo juu huenda ningekuwa nilishaandika makala hii
tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Lakini nilisita kuandika fursa hii mapema
pasipo kuwa na majibu ya maswali hayo kwa wasomaji. Leo nina majibu
hayo. Pia nikujulishe kuwa msimu wa kutafuta na kuandaa mashamba
tunaanza Agosti-Oktoba na upandaji ni Novemba-Desemba hadi Januari kwa
wanaokuwa wamechelewa.
Sifa
kubwa ya ujasiriamali ni kufanya huduma kwa watu wengine, yaani kutafuta
mahitaji, shida, matatizo na matamanio yao na kuwatimizia. Kama
alivyosema mfanyabiashara mmoja wa Kimarekani, Zig Ziglar; "Utapata
unachokitaka ikiwa utawasaidia watu wengine wengi kupata wanachokitaka".
Katika
kuwasaidia wengine ili wawekeze katika biashara hii ya mashamba ya miti
ninaongozwa na mambo makubwa mawili ninayotaka kuona yakitimia. Mosi,
mimi na wewe tuungane na serikali na dunia nzima katika kupambana na
mabadiliko ya tabia nchi kwa kupanda miti mingi.
Pili,
nataka nikusaidie wewe ambaye kila siku nimekuhamasisha ufikirie
biashara na uwekezaji, uchukue hatua ya kuwekeza ili ujikwamue kiuchumi
kwa kuvuna mamilioni. Moja ya ndoto nilizonazo duniani ni kuzalisha na
kuendeleza wafanyabiashara na wawekezaji wapya kwa maelfu hadi naingia
kaburini. Huo ndiyo wito wangu duniani.
Ili
kutimiza ndoto yangu hiyo, nimeweka utaratibu ufuatao utakaohakikisha
kila mwenye ndoto, kiu na hamasiko la kuwekeza kwenye kilimo cha miti
anafanikiwa. Kupitia mfumo wa biashara zangu nimeanzisha kitengo maalumu
kijulikanacho kama Fresh Farms (T).
Kazi
yangu kupitia kitengo hiki itakuwa ni kukupa ushauri wa kibiashara,
kukutafutia maeneo ndani ya Mkoa wa Iringa kwa ekari unazotaka,
kukuandalia hayo mashamba, kukupandia hiyo miti na kusimamia utunzaji wa
shamba katika hatua za awali na hata baadaye. Jisikie huru wakati
wowote kuwasiliana nami kwa ufafanuzi na msaada wa fursa hii.
Kwa
kutumia sheria, taratibu na tamaduni zote za wenyeji zinazohusiana na
umilikaji ardhi nitahakikisha nakusaidia ili ndoto yako itimie. Nadhani
kwa utaratibu huu ipo siku nami naweza kusimama na kujivunia mazao ya
watu waliokombolewa kivitendo kutokana na harakati zangu za kuelimisha
watu kuhusu ujasiriamali, uchumi na biashara.
Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi kupitia uwekezaji!
No comments:
Post a Comment