Saturday, June 22, 2013

NKAMIA ACHAFUA HALI YA HEWA BUNGENI/MJENGONI

1625 cb219Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM), kwa mara nyingine ameingia katika kashfa nzito akituhumiwa kutaka kumpiga Mbunge wa Viti Maalumu CUF, Moza Abeid ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa wiki ambapo imeelezwa kuwa Nkamia mbali na kutaka kumpiga mbunge huyo, pia alimtolea matusi mazito ya nguoni (gazeti hili haliwezi kuandika).
Kwa mara ya kwanza mbunge huyo aliingia katika kashfa baada ya kutoa kauli bungeni kuwa hazungumzi na mbwa, bali anazungumza na mwenye mbwa kabla ya kuingia katika mzozo na wahariri na baraza la habari aliposema kuwa Jukwaa la Wahariri na Baraza la Habari ni NGOs za kutafuta fedha.

Uchunguzi wa Mwananchi ambao umethibitishwa na Nkamia mwenyewe umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni kutokana na kuzomewa kwa Nkamia katika kampeni za uchaguzi mdogo Kata ya Dalai Wilaya ya Chemba.
Kwa mujibu wa wabunge mashuhuda ambao waliliona tukio hilo, ilielezwa kuwa Nkamia, ambaye pia ni mwandishi wa habari, alianza kumshushia matusi Moza wakiwa ndani ya Bunge hadi walipotoka nje alimfuata na kutaka kumpiga.
"Kweli pale jamaa yetu, alitia aibu, hata hivyo kusema kuwa alikuwa amelewa siyo kweli maana mimi namfahamu Nkamia vizuri ila ilikuwa ni hasira tu," alisema mmoja wa wabunge walioamua ugomvi huo.
Akizungumzia tukio hilo Moza, alisema kuwa wakati akitoka nje ya ukumbi, alipita karibu na kiti anachokaa Nkamia na ghafla akaitwa, lakini akashangazwa na kitendo cha kuanza kurushiwa matusi.
"Kweli Nkamia na mimi tunatoka wilaya moja, lakini siku ile nilishangaa alinitukana matusi ya nguoni kabisa ......... (anayataja), lakini mimi kule sikusema kitu hadi nilipotoka nje alinifuata na mimi hasira ilinishika nikaanza kumjibu akatupa vitabu ili aje anipige wabunge wenzake wakamkamata," alisema Moza.
Alisema kuwa chanzo cha matusi hayo ilikuwa ni tuhuma kwamba Nkamia alimtuhumu Moza kuwa aliandaa vijana katika Kata ya Dalai wakati wa kampeni za uchaguzi wa udiwani ili wamtukane.
"Hata hivyo, waliomwambia hivyo kwamba niliandaa vijana au nilimtukana walimdanganya kwani mimi wakati huo nilikuwa bungeni, lakini yeye ndiye aliyeniporomoshea matusi katika kampeni hizo na ushahidi wa sauti ninao," alisisitiza Moza.
Kwa upande wake Nkamia, ambaye kabla ya kuwa mbunge alikuwa mtumishi wa Serikali katika Shirika la Tanzania Broadcasting Corporation (TBC) alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini alikanusha kuingia bungeni akiwa amelewa kama ilivyoaminika na watu.
Nkamia alitoa sababu za ugomvi huo kuwa ni kutokana na taarifa kuwa Moza aliandaa kikosi cha vijana wahuni kulishambulia gari la Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kuwazomea viongozi wake akiwemo yeye.

No comments:

Post a Comment