Arusha.Diwani wa Chadema Kata ya Kiranyi wilayani Arumeru mkoani
Arusha,Patrick Bille ameeleza kwa masikitiko jinsi bomu lilivyomlipua na
kusema kwamba awali akiwa karibu na jukwaa kuu aliona mfuko wa plastiki
ukipepea angani ambao ulitua chini ya jukwaa na kisha kulipuka.
Bille
ambaye kwa sasa anaishi akiwa na vipande vya chuma mwilini alisema
kuwa,kabla ya mfuko huo kutua ardhini alifikiri ni jiwe kwa kuwa alikuwa
mita tatu tu kutoka ulipotua lakini ghafla alishangaa kuona ukilipuka
na kumjeruhi vibaya.
“Wakati nikiwa pale jukwaani niliona mfuko
mweusi ukipepea angani nikahisi ni jiwe limerushwa ghafla ulitua karibu
na nilipokuwa lakini nikasikia mlipuko ghafla na kuna vyuma vikanirukia
,”alisimulia Bille.
Hata hivyo,alisema kuwa hakumwona mtu
aliyerusha mfuko huo lakini ulitokea upande wa Baa ya Soweto iliyokuwa
mkabala na jukwaa kuu upande wa Magharibi.
Akiendelea kusimulia
alisema kwamba mara baada ya mfuko huo kulipuka alipigwa na vipande vya
chuma katika eneo la kifua chake na mkono wa kulia na kisha kupoteza
fahamu na kujikuta akiwa hospitali ya Selian.
Hata hivyo,alisema
kuwa anakumbuka wakati akiwa jukwaani kulikuwa na amani ya kutosha na
neno la mwisho analolikumbuka lilitamkwa na Mwenyekiti wa
Chadema,Freeman Mbowe ambapo aliwataka watu wakichangie chama chao fedha
za kuwawezesha kumaliza uchaguzi salama.
“Pale jukwaani
nakumbuka kulikuwa na amani kabisa lakini nakumbuka neno la mwisho
alilosema mwenyekiti wangu kwamba watu wachangie fedha za kukisaidia
chama kishinde uchaguzi,”alisisitiza Bille
Diwani huyo kwa
unyonge alisema kuwa baaya kufikishwa hospitalini hapo madaktari
walimwambia ya kwamba ameonekana na vipande vya chuma mwilini ambavyo
vimeingia umbali wa inchi mbili na wanasubiria visogee ili viweze
kutolewa.
No comments:
Post a Comment