TUMEZOEA
kuanza siku kwa kunywa vinywaji moto kama vile kahawa au chai na hii
imekuwa ndiyo desturi ya maisha ya watu wengi duniani. Lakini siyo
lazima kuanza siku yako kwa kunywa vinywaji hivyo, ambavyo tafiti nyingi
zimeonesha chai na kahawa vikitumiwa kupita kiasi vinaweza kuwa na
athari kwa mtumiaji.
Katika
kuangalia njia mbadala na bora ya kufungua kinywa na kuanza siku
vizuri, imebainika kuwa glasi moja ya maji ya uvuguvugu
yaliyochanganywa na juisi ya limau kipande kimoja, yana faida kubwa
mwilini na yanafaa kutumiwa kama kifungua kinywa asubuhi.
Zifuatazo
ni baadhi ya faida kubwa za kunywa maji kwa kuchanganya na juisi ya
limau asilia kama zilivyoanishwa na kuthibitishwa na tafiti mbalimbali
za kisayansi:
HUSAIDIA USAGAJI CHAKULA: Maji ya uvuguvugu husaidia kuuamsha na
kuuchangamsha utumbo na maji ya limau hulainisha na kuondoa sumu yoyote
inayoweza kuwa imeganda kwenye utumbo na kuipeleka kweye njia ya haja
kubwa ili kutolewa kama uchafu.
HUONDOA SUMU KWENYE NGOZI NA MWILINI: Unywaji wa maji ya uvuguvugu
yaliyochanganywa na juisi ya limau husaidia sana kuondoa sumu na uchafu
kwenye ngozi kwa njia ya mkojo. Aidha, kiwango kingi cha Vitamin C
kilichomo kwenye juisi ya limau huondoa takataka zote za kwenye mwili na
damu, hivyo kuiacha ngozi yako safi, laini na nyororo.
HUIMARISHA KINGA YA MWILI: Kama tulivyoona hapo juu, limau lina
kiwango kingi cha Vitamin C ambayo ni muhimu katika kujenga kinga ya
mwili na huzuia magonjwa ya mafua na kikohozi. Halikadhalika limau lina
kiwango kingi cha ‘potasiamu’ ambayo huamsha ubongo na kudhibiti
shinikizo la damu.
HUONDOA ULEVI WA KAHAWA: Kuna watu wameshazoea kunywa kahawa kila
siku na kuwa kama ulevi, kwani wanapokosa kunywa huwa kama wagonjwa,
lakini kwa kunywa maji na limau hali hiyo ya ‘uteja’ huondoka na
kujisikia huru na mchangamfu.
HUSAIDIA KUPUNGUZA UZITO: Limau pia lina kiwango kingi cha
kirutubisho aina ya kamba lishe (pectin fiber) ambacho ukikila
kinakufanya ujisikie kushiba. Hivyo maji haya ni mazuri sana kwa watu
wenye kuhitaji kupunguza uzito au kuimarisha uzito walionao.
MAMBO YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZA
Hakikisha kiwango cha joto cha
maji utakayotumia kiwe cha kati, si ya moto wala baridi. Maji moto sana
siyo mazuri kwasababu yataua virutubisho vilivyomo kwenye limau na ya
baridi sana yanaweza kusumbua tumboni. Pia yawe maji safi na salama.
Ili
kuyalinda meno yako dhidi ya uchachu wa limau, pendelea kutumia mrija
kunyonyea maji hayo. Hakikisha unakamua juisi yako kutoka kipande cha
limau halisi na siyo juisi ya limau iliyosindikwa kwenye chupa.
Ukiwa
na mazoea ya kuanza siku yako kwa kunywa mchanganyiko huu wa maji na
juisi ya limau, afya yako itaimarika, hutapatwa na magonjwa kirahisi na
ngozi yako itakuwa laini na nyororo.
No comments:
Post a Comment